Vijana wa Kiafrika ishirini ambao biashara zao zinatoa suluhu bunifu zinazoendeleza ukabilifu wa mabadiliko ya tabianchi na unyumbufu wamepokea tuzo ya $100,000 kila mmoja kwa kushinda tuzo ya Shindano la Suluhu la Ukabilifu la Vijana wa Kiafrika la 2022-2023 (#YouthAdapt Challenge).
Tunapoinusuru Afrika, tunaunusuru ulimwengu; tunapounusuru ulimwengu, tunaunusuru kwa manufaa ya vijana wa sasa na wa kesho
Gislaine Matiedje Nkenmayi, kutoka Kameroon, alikuwa miongoni mwa vijana 10 wa Kiafrika walioshinda tuzo ya Shindano la #YouthAdapt mwaka 2021.
Bi. Nkenmayi anasimamia Muminta Holdings - kampuni ya kusindika bidhaa za kilizo iliyoko Buea, eneo la kusini magharibi mwa Kameroon. Kampuni hiyo inahusika na kukabiliana na maisha mafupi katika mikondo ya thamani ya mboga.
“$100,000 tulizopokea zilituwezesha kufanya kazi na wakulima wengi zaidi, kutoka wakulima wadogo 357 hadi zaidi ya 700, wengi wao wakiwa wanawake. Wakulima wenyewe wanawaajiri watu wengi zaidi,” anasema Bi. Nkenmayi.
“Tulianza biashara hii kwa sababu tuligundua kwamba wakulima wanawake wa mboga walikuwa wakipata hasara kuu za baada ya mavuno, wakati mwingine kufikia 90%, kwa sababu ya kukosa vifaa vya uhifadhi. Aidha mboga zao zilikauka kwa sababu ya ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Sasa wameanzisha vivugulio 10 nafuu kupitia kwa vyama vya ushirika vya wakulima ili kuhakikisha kwamba wakulima wanaweza kulima mwaka mzima.
“Na tuna mifumo ya unyunyiziaji maji inayoendeshwa kwa nguvu za jua inayosaidia kuyasukuma maji kutoka katika mapipa au visima hadi katika vivugulio.
Aidha vinatoa mafundisho ya ufundi wa baada ya mavuno kwa wakulima na kuwaunganisha na masoko mapya. Matokeo ni kwamba shirika hilo limefupisha kipidi baina ya uzalishaji na utashi.
“Wanawake wengi zaidi sasa wanajihusisha. Tumeongeza mazao ya kilimo, kuwawezesha wanawake wengi zaidi na kuimarisha ukabilifu wa tabianchi,” anasema Bi. Nkenmayi.
Wakiwa wamechaguliwa kutoka kwa washiriki 3,000, washindi hao 20 pia watapata ushauri na ukufunzi.
Sherehe hiyo ya kutoa tuzo ilifanyika tarehe 10 Novemba katika COP27 jijini Sharm El Sheikh, Misri. Washindi hao 20 walishiriki kupitia kiungo cha video.
Shabaha ya chini kabisa ni kwa Afrika kujilisha; shabaha kuu ni kwa Afrika kuulisha ulimwengu
Shindano hilo la #YouthAdapt linaandaliwa kwa ushirikiano wa (AfDB), (GCA) na UN (CIF) ili “kuimarisha ubunaji ajira endelevu kupitia usaidizi wa ujasiriamali na ubunifu unaoongozwa na vijana katika ukabilifu wa mabadiliko ya tabianchi na unyumbufu katika Afrika,” kulingana na AfDB.
Rais wa AfDB Akinwumi Adesina aliwapongeza washindi, nusu yao wakiwa wanawake, kwa kutoa suluhu bunifu kwa ukabilifu wa tabianchi na unyumbufu katika kilimo, miundomsingi, udhibiti wa taka miongoni mwa sekta nyinginezo.
Vijana wa Kiafrika wanastahili kuwa “Vuvuzela [pembe za kelele] kwa manufaa ya Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
“Tunainusuru Afrika, tunaunusurua ulimwengu; tunaunusuru kwa manufaa ya vijana wa leo na wa kesho,” Bw. Adesina alisema. “Shabaha ya chini kabisa, ni kwa Afrika kujilisha, shabaha kuu ni kwa Afrika kuulisha ulimwengu.”
Patrick Verkooijen, Afisa Mkuu Mtendaji wa Halmashauri ya utendaji ya GCA, alizungumza kuhusu “tanzia halisi ya tabianchi inayojitokeza katika Afrika.” alisema kwamba ni muhimu kwa mataifa tajiri kulisaidia bara hili, huku akisisitiza kwamba, “Athari ya mabadiliko ya tabianchi katika Afrika haitasalia katika Afrika; itasafiri ulimwenguni kote.”
Waziri wa Norway wa Maendeleo ya Kimataifa, Anne Beathe Tvinnereim, aliwapongeza vijana wa Kiafrika wajasiriamali kwa kupendekeza suluhu za tabianchi zilizobuniwa mahususi kukabili hali ya Afrika. “Ukabilifu unatokana na uhitaji, lakini pia unatoa fursa za ujasiriamali na ajira,” alisema.
Mmoja kati ya washindi wa mwaka huu Yvette Ishimwe wa Rwanda, aliitaja tuzo hiyo kama “fursa ya kubadilisha maisha. Itaiwezesha [biashara yake] kutoa maji zaidi ya kunywa kwa raia na kubuni nafasi za ajira.”
Kampuni ya Bi. Ishimwe, Iriba Water Group, inatoa suluhu la ukabilifu kwa mafuriko. Inayakusanya maji ya mvua kutoka kwa mapaa, inayatakasa na kuwagawia wanawake katika nchi yake.
Sherehe ya kwanza ya shindano la #YouthAdapt iliandaliwa mwaka jana katika COP26 jijini Glasgow, na kuwanufaisha vijana wajasiramali 10 katika biashara ndogondogo, ndogo na wastani.