±¬ÁϹ«Éç

Kama mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Sierra Leone itaendeleza amani, usalama na utawala bora barani Afrika

Get monthly
e-newsletter

Kama mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Sierra Leone itaendeleza amani, usalama na utawala bora barani Afrika

— asema Waziri wa Mambo ya Kigeni David Francis
Kingsley Ighobor
Afrika Upya: 
16 June 2023
Sierra Leone Ilichaguliwa Mwanachama asiye wa Kudumu wa Baraza la Usalama kwa 2024 - 2025.
Ikiwa huwezi kusoma sasa, sikiliza tu toleo la sauti: 
Sauti iko kwa Kiingereza.

Sierra Leone ilipata mafanikio makubwa tarehe 6 Juni ilipochaguliwa katika kiti kisicho cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2024 hadi 2025. Waziri wa Mambo ya Kigeni na Ushirikiano wa Kimataifa, Prof. David Francis alizungumza na Kingsley Ighobor kutoka Afrika Upya kuhusu maana ya tukio hilo kwa Sierra Leone na Afrika, na vipaumbele ambavyo nchi hiyo inakusudia kuendeleza wakati wa uongozi wake. Madondoo haya yafuatayo yanatokana na mahojiano hayo:

Je, mafanikio haya yana umuhimu gani kwa nchi yako, na pia kwa Afrika?

Leo ni siku muhimu kwa Sierra Leone. Tunarejea kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kitengo kisicho cha kudumu baada ya miaka 53. Kupigiwa kura na nchi 188 [kuna nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa] ni dhihirisho la heshima kwa Sierra Leone.

Sierra Leone haijulikani tena na hali yake tatizi kama zamani. Leo hii tunachukuliwa kuwa taifa huru, linaloendelea, linalojiamini na lenye uwezo.

Kama unavyojua Sierra Leone ni Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika ya mataifa 10 (C-10) kwa ajili ya mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Aljeria, mwanachama mwingine wa C-10, leo pia limechaguliwa katika kundi lisilo la kudumu la Baraza la Usalama. Hii ina maana kwamba mwaka 2024 na 2025, wanachama wawili wa C-10 watapaza sauti yetu ya pamoja ili kuendeleza na kutetea msimamo wa pamoja wa Afrika kwa ajili ya mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ni mambo gani yalichangia kutokuwepo kwa Siera Leone kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu, na taifa hili liliwezaje kurejea?

Kutokuwepo kwa Sierra Leone kunaweza kuhusishwa na sababu kadhaa, ikiwemo kipindi kigumu kilichokumbwa na vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe, utawala mbaya na serikali kushindwa kufanya kazi.

Unapokuwa katika kipindi cha utawala mbaya, usimamizi usiofaa wa kisiasa na kiuchumi na vita vya wenyewe kwa wenyewe, huna wakati wa kuja kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hakuna atakayekupigia kura kwa sababu hatakuheshimu.

Hata hivyo, nchi yetu iliweza kurejesha nafasi yake kupitia msururu wa hatua. Mikakati ya Umoja wa Mataifa na kikosi cha kulinda amani cha Afrika Magharibi, ECOMOG, ulitekeleza jukumu muhimu katika kusaidia Sierra Leone kujikwamua kutoka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kujijenga upya.

Tulipiga hatua za kukomesha vita na kuendeleza amani, sasa tuko katika harakati za kuimarisha demokrasia. Tunachukuliwa kama mfano wa mafanikio ya ujenzi wa amani baada ya vita na ujenzi wa taifa.

Mwaka 2018, Sierra Leone iliorodheshwa kama moja ya nchi fisadi zaidi ulimwenguni. Hata hivyo, kupitia juhudi thabiti, Sierra Leone iliweza kuboresha alama zake kwenye kipimo cha Shirika la Changamoto za Milenia ya Kudhibiti Ufisadi, kutoka 49% mwaka wa 2018 hadi 83%, mwaka wa 2022.

Kama Waziri wa Mambo ya Kigeni, nilihamasisha misheni zetu za kidiplomasia, haswa huko New York, Jeneva, Nairobi, Addis Ababa na Abuja, ili kutetea na kupata kiti cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Juhudi hizi zilikuwa na changamoto, hasa ikizingatiwa kuwa Nijeria pia ilikuwa ikiwania nafasi hiyo. Hata hivyo, Nijeria, chini ya uongozi wa Rais wa zamani Mohammadu Buhari, ilionyesha uungwana kwa kuiachia Sierra Leone fursa hiyo.

Ulitaja katika uzinduzi wa kampeni mwaka jana kwamba vipaumbele vyako vitakuwa kuendeleza amani na usalama, uwezeshaji wa wanawake na vijana, kushughulikia mageuzi ya tabianchi na mengine. Kwa wanawake na vijana, ni mipango gani uliyo nayo nyumbani inayoonyesha kujitolea kwako kwa malengo haya?

Tuna vipaumbele saba vya kimkakati lakini wacha niangazie wanawake na vijana. Serikali yetu inatambua umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu, hasa kuwapa kipaumbele wanawake na vijana. Huku wanawake wakijumuisha karibu asilimia 52 ya watu wetu, ni muhimu kuzingatia kuwawezesha.

Ili kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, tulipitisha Sheria ya kimsingi kuhusu Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake mwaka uliopita wa 2022. Sheria hii inahakikisha kiwango kisichopungua cha asilimia 30 kwa wanawake katika nyadhifa za kuchaguliwa, nyadhifa za kuteuliwa, na kupata mtaji wa kibinafsi kutoka kwa benki.

Juhudi kama hizo zimefanywa kuwawezesha vijana. Tumeunda fursa za mafunzo ya ujuzi na maendeleo kama vile Mashamba ya Kilimo ya Vijana ambapo vijana wanachangia usalama wa chakula na kupata elimu ya kiufundi.

Katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, tunalenga kubadilishana uzoefu wetu na wengine duniani.

Bado kuna maeneo mengi yenye matatizo barani Afrika. Katika miaka ya tisini, vita vya Liberia vilienea hadi Sierra Leone. Sasa Guinea, nchi nyingine jirani, iko katika mpito wa kisiasa kufuatia mapinduzi ya Septemba 2021. Je, unachangia vipi katika kurejesha demokrasia nchini humo?

Mapinduzi ya kijeshi ni tishio kwa amani, usalama na uthabiti wa kanda yetu ndogo. Kwa sasa, mamlaka za mpito ziko Mali, Burkina Faso na Guinea.

Hatuwezi kuruhusu Guinea kuathiriwa na mizozo mikubwa kwa sababu ya mizozo hiyo kutufikia au athari ya kuwa na vita karibu sana nawe, kama ninavyoizungumzia kila mara.

Rais Bio mwenyewe ametembelea Guinea, Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Umoja na Maendeleo [Col. Mamady Doumbouya] naye pia ametembelea Sierra Leone. Tumefikia makubaliano kwamba tutaunga mkono mchakato huo kwa kuelewa kwamba wataendelea kujitolea kwaÌý ajenda ya mpito ya ECOWAS [Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi].

Rais pia amekuwa Mali, na amenituma kama Mjumbe wake Maalum ili nishirikiane na uongozi wa Burkina Faso. Vivyo hivyo Rais wetu amekuwa Mali, na amenituma kama Mjumbe wake Maalum ili nishirikiane na uongozi wa Burkina Faso.

Je, una matumaini?

Kwa upande mmoja, ndiyo, lakini wakati huo huo, katika siasa, huwezi kuwa na uhakika. Jukumu letu ni kuwahimiza waendelee kujitolea kurejesha utawala wa kikatiba na kidemokrasia.

Kipimo cha Ugaidi Ulimwenguni cha 2023 kinarejelea eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kama kitovu cha ugaidi, kuzidi maeneo mengine. Je, unakusudia kutumiaje uanachama wako katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhamasisha nchi barani Afrika na kwa hakika washirika wako wa kimataifa kupambana na ugaidi katika bara hili?

Ugaidi katika eneo la Sahara ni tishio kwa amani, usalama na utulivu wa bara hili. Tunajua changamoto za ukosefu wa usalama nchini Mali na Burkina Faso.

Sierra Leone, ingawa haijaathiriwa moja kwa moja na shughuli za kigaidi, imekumbwa na historia ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na inaelewa matokeo mabaya ya ukosefu wa usalama.

Tutashirikiana na washiriki wote ndani ya mfumo wa ECOWAS na kupitia ushirikiano wa nchi mbili. Katika mazungumzo yangu na Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uingereza na wenzake wengine wa Ulaya, wakiwemo mawaziri wa mambo ya kigeni, tumeandaa pendekezo linalolenga kupambana na ugaidi katika eneo hili.

Hata hivyo, ni lazima pia kushughulikia chanzo cha ugaidi.

Ni nini kinachowasukuma watu wa kawaida katika eneo la Sahara kujihusisha na shughuli za kigaidi? Tunafikiria tuna ufahamu mzuri wa changamoto za tatizo hili.

Chanzo kikuu ni kubaguliwa, kunyang'anywa mali, umaskini, kunyimwa, kutengwa na michakato ya kiuchumi na kisiasa ndani ya nchi.

Ili kushughulikia masuala haya ipasavyo, ni muhimu kuweka kipaumbele kwa utawala wa kidemokrasia, ambapo watu binafsi wanaweza kutoa maoni yao kwa uhuru na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayoathiri maisha yao. Kushindwa huko kunawasukuma na kuwafanya wakubali itikadi kali kwa sababu hawana cha kupoteza.

Kama Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika wa wajumbe 10 wenye wajibu wa kutetea mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, je, sababu bora ya Afrika kutaka viti vingine zaidi katika baraza hilo ni ipi na hali halisi ya sasa ya kijiografia inasisitiza haja ya mageuzi hayo?

Sababu bora ya Afrika ni kwamba ulimwengu ulioanzisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa miaka 77 iliyopita ni tofauti sana na wa leo.

Huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanyiwa mageuzi mara moja, kuanzia 1963-1965, na kuongeza wanachama wake kutoka 11 hadi 15, Afrika iliendelea kuwa na uwakilishi wa chini katika kundi lisilo la kudumu na kutokuwa na uwakilishi katika kundi la kudumu.

Kushughulikia dhuluma za kihistoria na kutengwa kwa kanda nyingi za ulimwengu, pamoja na Afrika, ni sababu ya kimaadili na kisiasa.

Aidha, hali za kijiografia na kisiasa zimebadilika kwa kiasi kikubwa, hasa tangu tarehe 24 Februari 2022 [Urusi kuvamia Ukraine].

Wanachama wa P-5 [Nchi Tano katika nafasi ya Kudumu zinajumuisha Uchina, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani) wanachama wameonyesha nia ya kufanya mageuzi katika Baraza la Usalama, hasa kuleta kanda nyingine za dunia, ikiwemo Afrika. Hata hivyo, kuna cha mno.

Afrika ina msimamo mmoja, ambao taifa la Sierra Leone litaendeleza.

Tutatetea viti viwili katika kitengo cha kudumu, ikijumuisha haki yote pamoja na kura ya kipekee, ikiwa itadumishwa. Bila shaka, Sierra Leone na Aljeria zinaweza kuongeza ukaribu wao na wanachama wa P-5 ili kupaza sauti ya Afrika.

Uchaguzi unakaribia nchini Sierra Leone. Je, ushindi wako leo unasherehekewa na mirengo yote ya kisiasa nyumbani?

Kampeni za kuwania kiti hiki ziliungwa mkono na vyama vyote 11 nchini. Kama

Waziri wa Mambo ya Kigeni, nimefanya kazi na vyama vyote vya kisiasa bungeni. Wajumbe wa Kamati Teule ya Mambo ya Kigeni wameniunga mkono kikamilifu.

Hili linahusu Sierra Leone kama taifa; sio kupata alama za kisiasa.

Ìý