±¬ÁĎą«Éç

Wasifu wa ujana

Get monthly
e-newsletter

Wasifu wa ujana

Benedict Faustine Kikove wa Tanzania: “Balozi” wa haki za umma
Benedict Faustine Kikove
Afrika Upya: 
7 August 2019
Benedict Faustine Kikove
Benedict Faustine Kikove

Nilizaliwa mnamo1988, ambao ulikuwa wakati mgumu kiuchumi nchini mwangu. Tanzania ilikuwa ikipitia mpango wa marekebisho ya miundo yake ya kiuchumi (SAP).

Wakati huo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa zilihitaji mataifa yaliyokuwa na matatizo ya kiuchumi kuchukua ruzuku kwa mipango ya kijamii kabla ya kupata mikopo mipya. Kilikuwa pia kipindi cha shida nyingi za kimataifa kutokana na vita na mapinduzi ya serikali katika mataifa mengi barani Afrika, kusambaratika kwa Muungano wa Usovieti na kubomolewa kwa Ukuta wa Berlin. Umoja wa Mataifa ulihusika sana katika kusuluhisha shida hizi.

Mimi ni mtoto wa mfumo mpya wa ulimwengu. Ninaamini katika demokrasia na diplomasia ya kimataifa—kushirikiana kwa manufaa sawa ya binadamu. Wananiita Balozi nchini mwangu.

Nilisaidia kuanzisha vyama vya Umoja wa Mataifa katika shule nyingi nchini Tanzania. Kwa sasa mimi ndiye Makamu wa Rais wa Muungano wa Umoja wa Mataifa (UNA) nchini mwangu. Pia niko katika bodi ya wasimamizi wa Msichana Initiative, mpango wa kupigania haki za wasichana ulioanzishwa na mwanaharakati Rebecca Gyumi.

Kesi katika Mahakama Kuu

Mwaka wa 2016, Msichana Initiative iliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga ibara mbalimbali katika Sheria ya Ndoa ya 1971, ambayo ilikubalia wasichana kuolewa—kwa kibali cha wazazi wao pamoja na cha koti—wakiwa na umri wa miaka 14 au 15 tu.

Mwaka wa 2017 koti ilikubalia ombi letu, ikitangaza kwamba Sheria ya Ndoa sharti ifanyiwe marekebisho ili umri wa chini wa kuolewa uwe sawa kwa wavulana na wasichana. Hatua hiyo iliongeza umri wa kuolewa kwa wasichana hadi miaka 18. Ni ushindi tunaojivunia.

Hamu yangu katika maendeleo na harakati za kutetea haki za kibinadamu ilianza miaka 16 iliyopita, nilipokuwa katika shule ya upili, wakati mimi na wanafunzi wenzangu tulipofahamishwa kuhusu Umoja wa Mataifa na Kielelezo cha Umoja wa Mataifa (MUN). MUN ni kielelezo cha kuigiza kwa mamia ya maelfu ya wanafunzi duniani wanaokutana kujadili masuala ya kimataifa.

Pia nilipata fursa ya kukutana na mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa Eshila Maravanyika, ambaye anasimamia Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa nchini Tanzania. Nilijifunza mengi kuhusu shirika hilo kupitia kwa Bi. Maravanyika na ziara kadhaa kwa ofisi za Umoja wa Mataifa.

Kisha nikaamua kuanzisha chama ch Umoja wa Mataifa shuleni mwangu. Wanachama wetu walianza mpango wa kupanda miti shuleni na kuandaa mijadala kila mwezi kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Katika mwaka wangu wa mwisho katika shule ya upili, niliwaleta pamoja marafiki kuanzisha vyama vingine 27 vya Umoja wa Mataifa katika shule 27.

Nilifuzu elimu ya shule ya upili kwa alama bora zaidi na nikaenda kusomea Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Huku nikisomea shahada yangu ya kwanza, nilialikwa kila mara katika hafla mbalimbali shuleni na kwingineko kuzungumza, haswa na vijana. Katika harakati hizo nilikutana na viongozi mashuhuri, wakiwemo maRais wastaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki. Wote wanaendelea kunihamasisha na kunisaidia.

Kwa mara ya kwanza, mwaka huu nilialikwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York kuwakilisha mashirika yasiyo ya kiserikali katika Kikao Kikuu cha Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu, ambapo kwa mara ya kwanza, taifa letu liliwasilisha Ripoti ya Hiari ya Kitaifa kuhusu utekelezwaji wa wa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.

Muungano wa Umoja wa Mataifa (UNA), ambao mimi ni makamu wake wa Rais, ulishirikishaĚý michango ya mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ripoti ya kitaifa na ukasaidia kwa ubia kuandaa Jukwaa la Tanzania kuhusu Maendeleo Endelevu, ambalo lilijumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali 500 kutoka maeneo 14, pamoja na mashirika 70 ya vijana.

Mipango ya siku za usoni

Ningependa kujitosa katika siasa za kitaifa katika siku za usoni. Ningependa pia kuhutubia Kikao Kikuu cha Umoja wa Mataifa kwa niaba ya taifa langu siku moja.

Kwa sasa nitaangazia kupigia debe ushiriki muhimu wa vijana katika masuala ya maendeleo nchini Tanzania na kimataifa, na kuendelea kutetea haki za wasichana.

Ujumbe wangu kwa vijana wa Afrika ni, “Huu ni wakati wetu sasa na siku za usoni. Ni sharti tujihusishe na ujenzi wa taifa—hapana atakayetufanyia hilo.”

Ěý

Benedict Faustine Kikove
More from this author