±¬ÁĎą«Éç

Mradi wa UNICEF Liberia wadhihirisha uwezo wa barubaru katika kubadili maisha yao

Get monthly
e-newsletter

Mradi wa UNICEF Liberia wadhihirisha uwezo wa barubaru katika kubadili maisha yao

UN News
7 July 2020
By: 
Wasichana nchini Liberia wakifuatilia taarifa katika simu ya mkononi
UNICEF/Naftalin
Wasichana nchini Liberia wakifuatilia taarifa katika simu ya mkononi

Nchini Liberia, mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wa kuboresha maisha ya wasichana barubaru umekuwa na mchango mkubwa katika kushirikisha kundi hilo kwenye harakati za kuinua jamii zao na wakati huo huo kurejea shuleni.

Kwa kuzingatia kuwa barubaru ndio msingi wa mustakabali bora wa jamii, mradi huo umejikita kwenye maeneo ya makazi duni ya West Point na New Kru kwenye mji mkuu wa Liberia ,Monrovia.

Hawa Wanita Page ambaye ni mratibu wa programu hiyo ya barubaru anasema kuwa, “mradi huo ulipoanza mwaka 2011 baadhi ya wasichana walikuwa wanatumia madawa ya kulevya, wengine walikuwa makahaba na asilimia 70 walikuwa hawaendi shuleni. Changamoto kubwa ya mradi wetu ilikuwa ni jinsi ya kubuni mkakati ambao utawatoa wasichana hawa kutoka makazi duni hadi darasani.”

Ili kufanikisha mradi wao, iliamua kuwafuata barubaru hao kwenye makaziĚý yao badala ya kuwapeleka kwenye kituo cha UNICEF, ambapo kila asubuhi Bi. Page na timu yake walifika kwenye maeneo duni ya barubaru hao na kuzungumza nao kuhusu jinsi wanahatarisha maisha yao na vile ambavyo wanaweza kushirikiana kuboresha maisha yao.

“Mwanzoni ilikuwa ni vigumu sana kwa sababu hawakutuamini. Ilituchukua miezi mitatu hadi minne ya mwanzo kujenga imani,” anasema Bi. Page.

Baadhi ya changamoto wanazokumbana naoz ni pamoja na ukeketaji au FGM, mimba na ndoa katika umri mdogo, “kwa hiyo inabidi kuwa na eneo la faragha ambako unawaweka wasichana wa umri sawa kwenye chumba kimoja ili waweze kujadili masuala yanayowaathiri na kupata suluhu. Na wao wenyewe wanakuwa mstari wa mbele kupata majawabu.”

Mratibu huyo amesema kuwa baada ya kipindi cha miaka miwili, asilimia 70 ya wasichana walirejea shuleni na wanashiriki wao wenyewe kusongesha maisha yao.

“Mathalani wakati wa janga la Ebola, wasichana hawa walifundishwa jinsi ya kujikinga wao na familia zao dhidi ya ugonjwa huo na ndani ya siku 5 niliwaona hawa wasichana wakiwa mitaani, kwenye jamii zao wakielimisha kuhusu Ebola bila shinikizo lolote.”

UNICEF baada ya kuona uamuzi wa wasichana hao, iliamua kuwapatia mafunzo barubaru 500 wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao walifikisha ujumbe kwa kaya zaidi ya 8,000.

“Hatua hii imekuwa na manufaa makubwa, kwa hiyo ukiangalia wasichana hawa na ari yao na utayari wao na jinsi wamefanya kazi bila kupatiwa kiasi kikubwa cha fedha, nadhani hili ni eneo bora la kuweka msisitizo, iwapo tunaibua uwezo walio nao, wafahamu thamani ya kuwa barubaru na uwezo walio nao kubadili hii nchi, Liberia itakuwa pahala pazuri kwa watoto,” amesema Bi. Page.