Ϲ

Buriani Rais Pierre Nkurunziza, poleni warundi kwa msiba mkubwa -UN

Get monthly
e-newsletter

Buriani Rais Pierre Nkurunziza, poleni warundi kwa msiba mkubwa -UN

UN News
15 June 2020
By: 
Rais Pierre Nkurunziza wa Jamhuri ya Burundi, akihutubia kikao cha 66 cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo Septemba, 2011.
UN Photo/Lou Rouse
Rais Pierre Nkurunziza wa Jamhuri ya Burundi, akihutubia kikao cha 66 cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo Septemba, 2011.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amefariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo kwenye hospitali ya Karuzi iliyoko mji mkuu Bujumbura . Katika taarifa yake kufuatia kifo hicho iliyotolewa na msemaji wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamuza rambirambi kwa serikali ya Burundi, wananchi na familia ya kiongozi huyo.

Guterres amesisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kuisaidia serikali na watu wa Burundi wakati huu wakipambana na janga la COVID-19, na juhudi za nchi hiyo za kuendelea kuunda taifa imara, lenye mafanikio na mustakabali wenye amani kwa raia wote. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya la Umoja wa Mataifa, Burundi hadi sasa imethibitisha wagonjwa 83 wa corona na kifo kimoja.

Vyombo vya habari vimenukuu taarifa ya serikali ya Burundi ikisema kuwa, Rais Nkurunzinza aliugua na kupelekwa hospitali tarehe 7 mwezi huu wa Juni na hali yake kuimarika.

Hata hivyo mchana wa jana Jumatatu tarehe 8 hali ilibadilika na akapatiwa usaidizi wa mashine ya kupumua lakini alikata roho.

Tayari serikali ya Burundi imetangaza siku 7 za maombolezo na bendera itapepea nusu mlingoti.

Rais Nkurunziza alikuwa ni mtu wa aina gani

Na kutoka kwa Radio washirika Radio ya Taifa ya Burundi, RTNB, Ramadhan Kibuga anaangazia wasifu wa hayati Nkurunziza.

Rais Pierre Nkurunziza ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 55. Alizaliwa mwaka 1964 katika eneo la kaskazini la Ngozi.

Aliondoka Chuo kikuu akiwa Mkufunzi Msaidizi mwaka wa 1995 na kujiunga na kundi lililokuwa la waasi wakati huo na baadaye kuliongoza kundi hilo la CNDD/FDD hadi kufikia kwenye mazungumzo ya kusitisha vita na serikali mwaka 2003.

Katika Uchaguzi uliofuata wa mwaka 2005, Nkurunziza alikiongoza chama chake cha CNDD/FDD na kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu na hivyo kuwa rais wa Burundi katika kipindi cha miaka 15.

Hata Hivyo uchaguzi wa mwaka 2015 uligubikwa na machafuko makubwa baada ya upinzani kupinga muhula wake wa tatu wenye utata kwa madai kwamba ulikuwa kinyume na Makubaliano ya Arusha ya muongozo wa taifa hili.

Hivyo katika mwaka 2017, baada ya kupitishwa kwa katiba mpya , Rais Nkurunziza alitangaza kwamba hatogombea tena uraisnabaadaye kumtangaza mrithi wake Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye,ambaye amechaguliwa kuliongoza taifa hili kufuatia ushindimkubwa katika uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi mei mwaka huu, huku kuapishwa ilikuwa ikitarajiwa k ufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Hayati Nkurunziza atakumbukwa kwa mchango wake wa kimataifa hasa kuwapeleka walinda amani katika nchi za Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, kama sehemu ya vikosi vya Muungano wa Afrika pamoja na vile vya Umoja wa Mataifa.

Akituma vikosi hivyo wakati huo, Nkurunziza alisema "kila mara Jumuiya ya Kimataifa ilichangia kwa kiasi kikubwa katika kurejesha amani Burundi, hivyo ni wajibu kwa Burundi kulipa wema kwa kutunza amani katika maeneo mbalimbali duniani."