Ϲ

Ama hakika kiswahili kinaimarisha amani Mashariki mwa DRC

Get monthly
e-newsletter

Ama hakika kiswahili kinaimarisha amani Mashariki mwa DRC

UN News
Afrika Upya: 
5 July 2022
Na: 
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto wakazi wa Beni, nchini DRC.

Maadhimisho ya kwanza kabisa ya kimataifa ya lugha ya kiswahili duniani yanafanyika tarehe 7 mwezi huu wa Julai baada ya Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la Sayansi, Elimu na Utamaduni, UNESCO kupitisha siku hii mwezi Novemba mwaka 2021. Maudhui ya mwaka huu ni Kiswahili kwa ajili ya amani na ustawi.

Umoja wa Mataifa moja ya majukumu yake ni kuendeleza na kulinda amani mathalani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hususan mashariki mwa taifa hilo kumekuweko na mapigano yanayosababisha vifo vya raia, uharibifu wa mali, majeruhi na hata ukimbizi uwe wa ndani au wa nje.

Lugha ya Kiswahili imekuwa mhimili wa kufanikisha majukumu ya Umoja wa Mataifa kupitia walinda amani wake wanaotoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania na wakihudumu chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo,.

Eneo la Beni Kiswahili ni mhimili

Idhaa ya Kiswahili ilitaka kufahamu ni kwa vipi lugha ya kiswahili inasaidia kufanikisha majukumu yao ambapo Meja Amani Athumani ni Msaidizi wa Kamanda wa kikosi cha 9 cha Tanzania kinachohudumu MONUSCO, TANZBAT-9 mjini Beni, jimboni Kivu Kaskazini.

Meja Ramadhani anasema, “kikosi hiki kiko hapa kwa ajili ya ulinzi wa amani na asilimia kubwa ya wenyeji wa hapa Beni wanatumia lugha ya kiswahili na katika kuwasiliana na wananchi tunapata taarifa nyingi, kwa kupitia lugha ya Kiswahili.”

Amesema kwa kutumia kiswahili, wenyeji wanawapatia taarifa au habari kutoka sehemu zenye machafuko au mauaji na hiyo inawarahisishia kupeleka taarifa hizo makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa lugha ya kiingereza kwa sababu inakuwa ni rahisi kutafsiri kutoka Kiswahili kwenda kiingereza.

Walinda amani wa kikosi kipya cha Tanzania kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO.
Walinda amani wa kikosi kipya cha Tanzania kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wakiwa katika mkutano na wananchi huko Beni jimboni Kivu Kaskazini.
Picha: TANZBATT_8/Kapteni Tumaini Bigambo

Kiswahili ni amani

“Niseme tu lugha ya kiswahili inawakilisha amani. Kwa maana watu wanapofahamu kiswahili na kuweza kuwasiliana kwa lugha nyepesi basi naamini amani inaweza kupatikana kwa kutumia lugha ya kiswahili. Kiswahili kinaweza kutuunganisha na tukawa pamoja,” amesema Meja Ramadhani.

Meja Ramadhani akatumia methali ya kiswahili, “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu,” akimaanisha “tukiwa pamoja na tutakuwa na nguvu moja tutaendeleza kiswahili chetu, hata haya mambo ya kugombana, kufarakana kati ya nchi na nchi yatapungua kwa kutumia lugha hii ya kiswahili.”

Kwa upande wake Afisa Mteule daraja la I Raymond Ambayuu anasema, “lugha ya kiswahili ina umuhimu mkubwa sana kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa hapa Beni kwa sababu kinazungumzwa sana hapa.”

Kwa mujibu wa Ambayuu, “inatusaidia sana sana hasa kwa mataifa mbalimbali ambayo hayafahamu kifaransa au kiswahili, huwa wanatuomba sisi watanzania kuwasaidia kuwasiliana na wacongo ambao wanajua kiswahili.”

Kiswahili chaimarisha uhusiano kati ya walinda amani na wenyeji- Kambale

Katibu wa Chifu wa Sekta ya Rwenzori , Godfrey Kambale ambaye ni raia wa DRC wanaoshirikiana katika kazi na walinda amani wa MONUSCO anasema, awali wakati ujumbe huo ukiwa MONUC, walinda amani hawakufahamu kiswahili ilibidi mazungumzo yafanyike kupitia mkalimani.

“Lakini wakati ndugu zetu wanaongea kiswahili wamefika, japokuwa kuna matatizo fulani fulani ya kutoelewana kwa lugha, lakini kuna uhusiano mkubwa katika wananchi na MONUSCO ambao wanazungumza kiswahili. Kuna uhusiano zaidi na askari wanaozungumza kiswahili kuliko wale waliokuwa na tatizo la kuzungumza na wenyeji," amesisitiza Bwana Kambale.

Ameongeza kuwa kama wananchi wana shida yoyote iwe ya usalama au maendeleo wanaweza kuzungumza moja kwa moja na walinda amani badala ya kusubiri mkalimani.

“Kiswahili kinatusaidia sana kunapokuwa na tatizo,”amesema JAnvier Paluku, afisa kiungo wa jamii na walinda amani akiongeza kuwa wenyeji wana lugha zao kama kinande au kitalinda lakini kiswahili ni lugha ya kawaida hapa ni lugha ya mawasiliano na ni lugha inayounganisha makabila yote hapa.