Ilikuwa ni sherehe ya kufana kwenye kituo cha Baraza Media Lab jijini Nairobi, Kenya wakati Africa Podfest ikizinduliwa tarehe 12 Februari ili kuadhimisha Siku ya Podkasti ya Afrika mwaka huu- siku iliyotengwa ili kusherehekea wanapodkasti wakuu barani, na wale wanaoibukia.
Siku hii iliyozinduliwa mwaka 2020, ni ya kusherehekea kufanya podkasti barani Afrika, bara ambalo limeikumbatia zana hio maalum kwa kusimulia hadithi.
Kilele cha sherehe za mwaka huu kilikuwa ni uzinduzi wa Podkasti ya Afrika Upya - kipindi cha Idara ya Umoja wa Mataifa cha Mawasiliano ya Dunia (DGC).
Katika eneo la tukio - SemaBOX, studio ya wataalamu wa podkasti na kituo cha kukuza podkasti - ilirusha chengechenge hewani huku watu waliokuwepo wakishangilia uzinduzi wa podkasti hiyo. Kutokana na vikwazo vya Uviko-19, tamasha hilo lilikuwa ni mseto – ushiriki wa ana kwa ana na kwa kupitia mtandao.
Sandra Macharia, Mkuu wa Kitengo cha Afrika katika DGC, alisema Podkasti hiyo ya Afrika Upya, ambayo iliongezwa kwenye zana za mawasiliano za kitengo hicho ilikuwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza na kufanya majukwaa yake ya kidijitali kuwa anuai ili kufikia watu wengi zaidi.
"Ni ya sauti, inavutia sana na ni njia nzuri kwetu kufikia hadhira mpya kuhusu mada zinazohusu Afrika. Mada ambazo tunazichagua makusudi ili kuendeleza sauti za waafrika ambao wanafanya kazi katika bara hili na hadithi ambazo ni halisi, zinazohamasisha na kutoa matumaini kuhusu Afrika," Bi. Macharia alisema wakati wa uzinduzi.
Kipindi cha kwanza kati ya mfululizo wa vipindi vitatu kilichozinduliwa kinamwangazia Dkt. Joy Kategekwa, mtaalamu wa sheria ya biashara na sera katika Mpango wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP), ambaye ni mmoja wa wasanifu wa Makubaliano ya Eneo la Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA). Anajadili masuala yanayohusiana na biashara huru barani Afrika na kubainisha yanayowezekana? kutokana na mkataba huo wa biashara kwa maisha ya watu barani.
"Podkasti ya Afrika Upya inaangazia maendeleo ya Afrika kwa mtazamo wa watu wanaoishi na kufanya kazi ndani na kwa ajili ya bara hili," asema Nanette Braun, kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kimkakati katika DGC. "Inaangazia kazi za watu na taasisi kupitia hadithi zinazolenga kutoa muafaka kwa safari ya Afrika kijamii, kiuchumi na kisiasa."
Podkasti hii ni nyongeza kwa mifumo mingine ya mawasiliano ambayo Afrika Upya inatumia kusimulia hadithi za Afrika kuhusu maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Podkasti yetu inaongezea makala zilizopo za sauti na majukwaa mengine ya Afrika Upya yanayochangia katika kukidhi mahitaji ya maudhui ya ukweli na ya usawa kuhusu bara hili,” anaongeza Bi. Macharia.
Afrika Podfest iliasisiwa kwa pamoja na Bi. Josephine Karianjahi na Bi. Melissa Mbugua, ambao pia ndio walikuja na wazo la kufanya Siku ya Podkasti ya Afrika.
Hakika, utafiti uliofanywa mwaka jana uligundua kwamba waafrika wanasikiliza zaidi podkasti zilizozalishwa barani Afrika, na wanatafuta maudhui ya kuburudisha na kufahamisha.
"Mataifa makuu matatu ni Kenya, Nigeria na Afrika Kusini. Kadhalika, tuligundua kwamba nchi nyingine kama Zambia, Misri na nyingine zinakuza jumuiya zao na podkasti ambazo zinatengeneza," alisema Bi.Karianjahi.
Kuendelea kukua kwa mtandao na kupatikana kwa simu za mkononi barani kumesaidia ukuaji wa idadi ya watu wanaosikiliza podkasti.
Kaulimbiu katika maadhimisho ya 3 ya Podkasti ya Afrika ilikuwa ni "Uhuru wa Kufanya Podkasti " na yaliona mamia ya wanapodkasti wa Afrika walio barani na ughaibuni wakishiriki mtandaoni. Walishiriki uzoefu wao wa kufanya podkasti na jinsi ilivyomaanisha kwao na kwa wasikilizaji wao.
Waliohudhuria walisikiliza baadhi ya podkasti zinazokadiriwa kuwa bora zaidi barani Afrika, pamoja na za wale wanaoibuka kwenye eneo podkasti barani.
Bi. Khayriyyah Muhammad Smith, mwanapodkasti kutoka Marekani alizungumza kuhusu uwezo wa podkasti kuleta sauti za jamii zilizotengwa katika mazungumzo ya kila siku.
Podkasti ya Bi. Smith yenye jina Leta Kiti Chako-'Bring Your Own Chair' kwa mfano, huangazia wanawake ambao asili yao si weupe. "Tunawapa fursa ya kusimulia hadithi zao wenyewe kwa maneno yao wenyewe." Bi. Smith ambaye alikuwa miongoni mwa wageni wa kwanza wa tukio hilo alisema.
Kikosi cha shirika la utangazaji la uingereza-BBC World Service, ambacho kinaendesha podkasti ya Ana kwa Ana na Afrika kila siku - 'Africa Daily Live' kilizungumza kuhusu ni kwa nini mojawapo ya vituo vya redio vinavyoongoza duniani vingepanua wigo wao na kuanza kufanya podkasti.
Mwandishi na msomaji wa habari wa BBC Alan Kasujja aliwazungumzia waafrika kama wasimuliaji wakubwa wa hadithi, wakiwa na desturi ya simulizi ya mdomo. Alisema kutokana na kuja kwa podkasti, waafrika wengi zaidi sasa watakua na uhuru wa kusimulia hadithi zao wenyewe kwa lugha ambazo ni rahisi kwao kuzungumza.
"Ni uwezo mpya uliopatikana, wa kuzungumza ukweli wako. Mtumie uwezo huo, kuna hadithi nyingi sana huko nje," alisema Bw. Kasujja.
Mtayarishaji vipindi wa BBC, Victoria Uwonkunda, alisema kwamba kuna mustakabali kwa wanawake katika kufanya podkasti kwa kuwa ni nafasi salama kwao.
"Kuwa wewe, na kumbuka podkasti ni za kibinafsi sana kwa hivyo ni mahali pazuri pa kuzungumza kwa uhuru," alisema.
Mtandaoni, tunataka kuelewa waafrika wanatoa podkasti kuhusu nini na kaulimbiu ya siku ilimaanisha nini.
Mwanapodkasti wa Naijeria Bw. Rodney Omeokachie, mwandaaji wa podkasti ya ‘The Young God’ alisema kwamba anafurahia kuweza kujieleza kwa uhuru na bila woga.
“Uhuru ni hali ya kihisia, kila ninapobofya kitufe cha kurekodi, huyo ni mimi nikiwa huru,” aliiambia Afrika Upya.
Nnamdi Okaa, anayeishi nchini Canada, almaarufu kama Mista Dre, mmoja wa waandaaji na mtengenezaji wa podkasti ya ‘Backyard Bants’ alisema kwamba kwake kuwa huru ni kuwa na uwezo wa kukaa ughaibuni akiwa na jukwaa lake binafsi la kujieleza bila kuhukumiwa.
Changamoto, hata hivyo, zinabaki kwa wale wanaotegemea kuanzisha podkasti. Hizi ni pamoja na gharama za juu za data za mtandao wa simu katika nchi nyingi za Afrika, na vilevile gharama ya juu ya vifaa vinavyoweza kumpa mtu sauti nzuri na ubora wa kiufundi.
Licha ya changamoto hizi, wanapodkasti wengi barani Afrika wameweza kutengeneza fedha kutokana na podkasti.
Kwa hivyo bado unasubiri nini?